About Script
Surah At-Taghabun ( Mutual Loss & Gain )

Swahili

Surah At-Taghabun ( Mutual Loss & Gain ) - Aya count 18

يُسَبِّحُ لِلَّهِ مَا فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَمَا فِى ٱلْأَرْضِ ۖ لَهُ ٱلْمُلْكُ وَلَهُ ٱلْحَمْدُ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍۢ قَدِيرٌ ﴿١﴾

Kinamtakasa Mwenyezi Mungu kila kilichomo katika mbingu na katika ardhi. Ufalme ni wake, na sifa njema ni zake. Na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

هُوَ ٱلَّذِى خَلَقَكُمْ فَمِنكُمْ كَافِرٌۭ وَمِنكُم مُّؤْمِنٌۭ ۚ وَٱللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٢﴾

Yeye ndiye aliye kuumbeni. Miongoni mwenu yupo aliye kafiri, na yupo aliye Muumini. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.

خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ بِٱلْحَقِّ وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ ۖ وَإِلَيْهِ ٱلْمَصِيرُ ﴿٣﴾

Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na akakupeni sura, na akazifanya nzuri sura zenu. Na marudio ni kwake.

يَعْلَمُ مَا فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُسِرُّونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ۚ وَٱللَّهُ عَلِيمٌۢ بِذَاتِ ٱلصُّدُورِ ﴿٤﴾

Anajua viliomo katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliomo vifuani.

أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَبَؤُاْ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ مِن قَبْلُ فَذَاقُواْ وَبَالَ أَمْرِهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌۭ ﴿٥﴾

Kwani haikukujieni khabari ya walio kufuru kabla, wakaonja matokeo mabaya ya mambo yao? Na wao wana adhabu iliyo chungu.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُۥ كَانَت تَّأْتِيهِمْ رُسُلُهُم بِٱلْبَيِّنَٰتِ فَقَالُوٓاْ أَبَشَرٌۭ يَهْدُونَنَا فَكَفَرُواْ وَتَوَلَّواْ ۚ وَّٱسْتَغْنَى ٱللَّهُ ۚ وَٱللَّهُ غَنِىٌّ حَمِيدٌۭ ﴿٦﴾

Hayo ni kwa kuwa walikuwa wakiwajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, nao wakasema: Hivyo binaadamu ndio atuongoe? Basi wakakufuru, na wakageuka upande. Mwenyezi Mungu akawa hana haja nao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, si mhitaji, naye ni Msifiwa.

زَعَمَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوٓاْ أَن لَّن يُبْعَثُواْ ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّى لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٌۭ ﴿٧﴾

Walio kufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Naapa kwa Mola wangu Mlezi! Hapana shaka mtafufuliwa, na kisha hapana shaka mtaambiwa mliyo yatenda. Na hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.

فَـَٔامِنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ وَٱلنُّورِ ٱلَّذِىٓ أَنزَلْنَا ۚ وَٱللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌۭ ﴿٨﴾

Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru tuliyo iteremsha. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.

يَوْمَ يَجْمَعُكُمْ لِيَوْمِ ٱلْجَمْعِ ۖ ذَٰلِكَ يَوْمُ ٱلتَّغَابُنِ ۗ وَمَن يُؤْمِنۢ بِٱللَّهِ وَيَعْمَلْ صَٰلِحًۭا يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّـَٔاتِهِۦ وَيُدْخِلْهُ جَنَّٰتٍۢ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدًۭا ۚ ذَٰلِكَ ٱلْفَوْزُ ٱلْعَظِيمُ ﴿٩﴾

Siku atakayo kukusanyeni kwa ajili ya Siku ya Mkusanyiko; hiyo ni siku ya kupunjana. Na anaye muamini Mwenyezi Mungu na akatenda mema, atamfutia maovu yake, na atamuingiza katika Mabustani yenye kupitiwa kati yake na mito, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

وَٱلَّذِينَ كَفَرُواْ وَكَذَّبُواْ بِـَٔايَٰتِنَآ أُوْلَٰٓئِكَ أَصْحَٰبُ ٱلنَّارِ خَٰلِدِينَ فِيهَا ۖ وَبِئْسَ ٱلْمَصِيرُ ﴿١٠﴾

Na walio kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ni watu wa Motoni, watadumu humo milele. Na hayo ndiyo marudio mabaya.

مَآ أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ ٱللَّهِ ۗ وَمَن يُؤْمِنۢ بِٱللَّهِ يَهْدِ قَلْبَهُۥ ۚ وَٱللَّهُ بِكُلِّ شَىْءٍ عَلِيمٌۭ ﴿١١﴾

Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu huuongoa moyo wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

وَأَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ ۚ فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَإِنَّمَا عَلَىٰ رَسُولِنَا ٱلْبَلَٰغُ ٱلْمُبِينُ ﴿١٢﴾

Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Mkigeuka, basi hakika juu ya Mtume wetu ni kufikisha (Ujumbe wake) kwa uwazi tu.

ٱللَّهُ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ وَعَلَى ٱللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ ٱلْمُؤْمِنُونَ ﴿١٣﴾

Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Na juu ya Mwenyezi Mungu nawategemee Waumini.

يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِنَّ مِنْ أَزْوَٰجِكُمْ وَأَوْلَٰدِكُمْ عَدُوًّۭا لَّكُمْ فَٱحْذَرُوهُمْ ۚ وَإِن تَعْفُواْ وَتَصْفَحُواْ وَتَغْفِرُواْ فَإِنَّ ٱللَّهَ غَفُورٌۭ رَّحِيمٌ ﴿١٤﴾

Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.

إِنَّمَآ أَمْوَٰلُكُمْ وَأَوْلَٰدُكُمْ فِتْنَةٌۭ ۚ وَٱللَّهُ عِندَهُۥٓ أَجْرٌ عَظِيمٌۭ ﴿١٥﴾

Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.

فَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ مَا ٱسْتَطَعْتُمْ وَٱسْمَعُواْ وَأَطِيعُواْ وَأَنفِقُواْ خَيْرًۭا لِّأَنفُسِكُمْ ۗ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِۦ فَأُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلْمُفْلِحُونَ ﴿١٦﴾

Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo, na sikieni, na t'iini, na toeni, itakuwa kheri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio walio fanikiwa.

إِن تُقْرِضُواْ ٱللَّهَ قَرْضًا حَسَنًۭا يُضَٰعِفْهُ لَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَٱللَّهُ شَكُورٌ حَلِيمٌ ﴿١٧﴾

Mkimkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, atakuzidishieni mardufu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa shukra, Mpole.

عَٰلِمُ ٱلْغَيْبِ وَٱلشَّهَٰدَةِ ٱلْعَزِيزُ ٱلْحَكِيمُ ﴿١٨﴾

Mwenye kujua siri na dhaahiri, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Quran For All V5